UFUNGUZI WA MAKTABA MPYA UDSM

Campus Admin 2018-11-26 10:57:36 Notice Board

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinapenda kuwaalika wanajumuiya wote wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na umma kwa ujumla kushiriki katika ufunguzi wa Maktaba Mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam utakaofanyika siku ya Jumanne tarehe 27 Novemba 2018 kuanzia saa 2:00 asubuhi mpaka saa 6:30 mchana katika eneo la Maktaba mpya, Kampasi ya Mwalimu Julius Nyerere, Mlimani. Mgeni Rasmi katika ufunguzi huo atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Maktaba hii Mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam imejengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kupitia Kampuni ya Ujenzi ya Jiangsu Jiangdu kutoka China. Mradi umejumuisha majengo mawili, moja la Maktaba yenyewe na lingine la Taasisi ya Confucius ambayo imekuwa ikifundisha lugha na tamaduni za Kichina kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Watanzania wengine. Majengo yote mawili yanachukua eneo la mita za mraba takribani 20,000. Ndani ya Jengo la Maktaba kuna maeneo mbalimbali, yakiwa ni pamoja na sehemu za kuwekea makasha ya vitabu, maeneo ya kusomea vitabu na vitabu-pepe, ofisi za wafanyakazi na ukumbi wa kisasa wa mihadhara. Maktaba hii ina uwezo wa kukalisha wasomaji wapatao 2,100 kwa wakati mmoja na makasha yenye uwezo wa kuweka vitabu 800,000. Pia Maktaba hii mpya ina ukumbi wa mikutano wenye uwezo wa kukaa watu 600. Maktaba mpya itasaidia sana kupunguza uhaba wa eneo na vifaa vya kusomea wanafunzi kwani ina vifaa na kompyuta za kisasa zenye programu za kuweza kupata machapisho mbalimbali duniani. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinawaalika wadau wote wa elimu, Jumuiya ya Wahitimu, Viongozi wa Serikali, wadau wa maendeleo, mabalozi, viongozi wa kisiasa, viongozi wa vyama vya kiraia, waandishi wa habari na wananchi wote kwa ujumla kushiriki katika tukio hili muhimu kwa Chuo chetu na kwa maendeleo ya elimu ya juu nchini.